Biblia kwa picha

Nyumbani › Agano la Kale › Mwanzo

Mwanzo 22
Kutolewa kwa Isaka

Sura ya ishirini na mbili inasimulia jaribu kubwa kuliko yote la Abraham: Mungu anamwambia amtoe mwanawe Isaka kama sadaka juu ya mlima katika nchi ya Moria. Abraham anatii, lakini dakika ya mwisho malaika wa Yahwe anamzuia, na kondoo mume aliyenaswa pembe zake kichakani anatolewa badala ya Isaka. Kisha Mungu anafanya upya ahadi yake ya uzao usiohesabika.

Maandiko: Biblia Takatifu, Unlocked Literal Bible, © 2019, CC BY-SA 4.0. Vichwa, utangulizi na picha: Imago Biblia.

Mistari 1–5

Kuondoka alfajiri

Ikawa kwamba baada ya mambo hayo Mungu akampima Abraham. Akamwambia, “Abraham!” Abraham akasema, “Mimi hapa.”

Kisha Mungu akasema, “Mchukue mwanao, mwanao wa pekee, umpendaye, Isaka, na uende katika nchi ya Moria. Mtoe kama sadaka ya kuteketezwa mahali pale juu ya moja ya milima hiyo, ambayo nitakwambia.”

Kwa hiyo Abraham akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukuwa vijana wake wawili, pamoja na Isaka mwanawe. Akakata kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akapanga safari kwenda mahali ambapo Mungu alimwambia.

Siku ya tatu Abraham akatazama juu na akaona mahali pakiwa mbali.

Abraham akawambia vijana wake, “kaeni hapa pamoja na punda, mimi pamoja na Isaka tutakwenda pale. Tutaabudu na kisha tutarudi hapa penu.”

Alfajiri mbele ya hema, Abraham na kijana Isaka wanapakia kuni juu ya punda; watumishi wawili wanasubiri wakiwa na fimbo.

Mistari 6–8

“Mungu mwenyewe atatupatia mwanakondoo”

Ndipo Abraham akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa akaziweka juu ya Isaka mwanawe. Mkononi mwake akachukua moto na kisu; na wote wawili wakaondoka pamoja.

Isaka akazungumza na Abraham baba yake akisema, “Baba yangu,” naye akasema, “ Ndiyo mwanangu.” Akasema, “Tazama huu ni moto na kuni, lakini yuko wapi mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”

Abraham akasema, “Mungu mwenyewe atatupatia mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, mwanangu.” Kwa hiyo wakaendelea, wote wawili pamoja.

Kwenye njia ya mlimani, Isaka amebeba kuni mgongoni na kumtazama baba yake, aliyeshika chungu cha makaa na kuweka mkono begani mwake; chini watumishi wanasubiri na punda.

Mistari 9–12

Malaika anamzuia Abraham

Walipofika mahali ambapo Mungu alikuwa amemwambia, Abraham akajenga madhabahu pale na akaweka kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe, na akamlaza juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.

Abraham akanyoosha mkono wake akachukua kisu ili kumuua mwanawe.

Ndipo malaika wa Yahwe akamwita kutoka mbinguni na kusema, “Abraham, Abraham!” naye akasema, “Mimi hapa.”

Akasema, “usinyooshe mkono wako juu ya kijana, wala usifanye jambo lolote kumdhuru, kwa kuwa sasa najua unamcha Mungu, kwa kuona kuwa hukumzuilia mwanao, mwanao wa pekee, kwa ajili yangu.”

Juu ya mlima, Abraham amepiga magoti akiinua mkono kuelekea nuru inayopenya mawingu; Isaka ameketi juu ya madhabahu ya mawe akitazama mbinguni, na kisu kiko chini.

Mistari 13 na 14

Kondoo mume kichakani

Abraham akatazama juu na tazama, nyuma yake kulikuwa na kondoo mume amenaswa pembe zake kichakani. Abraham akaenda akamchukua kondoo na akamtoa kama sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

Kwa hiyo Abraham akapaita mahali pale, Yahwe atatoa,” na panaitwa hivyo hata leo. “Juu ya mlima wa Yahwe itatolewa.”

Karibu na madhabahu, Abraham na Isaka wanaona kondoo mume mwenye pembe zilizopinda amenaswa katika kichaka cha miiba.

Mistari 15–19

Kama nyota na mchanga

Malaika wa Yahwe akamwita Abraham kwa mara ya pili kutoka mbinguni

na kusema - Hiki ni kiapo cha Yahwe, “Kwa ajili ya nafsi yangu nimeapa kwamba kwa kuwa umefanya jambo hili, na hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,

hakika nitakubariki na nitakuzidishia uzao wako kama nyota za angani, na kama mchanga ulioko kwenye ufukwe wa bahari; na uzao wakowatamiliki lango la adui zao.

Kupitia uzao wako mataifa yote ya dunia watabarikiwa, kwa sababu umetii sauti yangu.”

Kwa hiyo Abraham akarejea kwa vijana wake, na wakaondoka wakaenda pamoja Beerisheba, hivyo akakaa Beerisheba.

Jioni, Abraham na Isaka wanashuka mlimani kando kwa kando chini ya nyota za kwanza; kwa mbali ufukwe wa bahari unang'aa, na watumishi wanafuata na punda.

Mistari 20–24

Habari za Nahori

Ikawa kwamba baada ya mambo haya ambayo Abraham aliambiwa, “Milka amemzalia pia watoto, ndugu yako Nahori.”

Hawa walikuwa ni Usi mzaliwa wa kwanza, Busi ndugu yake, Kemueli aliye mzaa Aramu,

Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu, na Bethueli.

Bethuel akamzaa Rebeka. Hawa walikuwa ni wale watoto wanane ambao Milka alizaa kwa Nahori, ndugu yake na Abraham.

Suria wake, ambaye aliitwa Reuma, pia akamzaa Teba, Gahamu, Tahashi, na Maaka.

Chini ya mti mkubwa, msafiri mwenye vumbi anahesabu kwa vidole mbele ya Abraham aliyeketi na Isaka aliyesimama karibu naye.