Biblia kwa picha

Nyumbani › Agano la Kale › Mwanzo

Mwanzo 2
Bustani ya Edeni

Sura ya pili inaanza na pumziko la Mungu siku ya saba, kisha inasimulia tena uumbaji kwa karibu zaidi. Yahwe Mungu anamuumba mtu kwa mavumbi, anapanda bustani katika Edeni na kumuumba mwanamke, ili mtu asiwe peke yake.

Maandiko: Biblia Takatifu, Unlocked Literal Bible, © 2019, CC BY-SA 4.0. Vichwa, utangulizi na picha: Imago Biblia.

Mistari 1–3

Pumziko la Mungu

Kisha mbingu na nchi zilimalizika, na viumbe hai vyote vilivyo jaza mbingu na nchi.

Siku ya saba Mungu alifikia mwisho wa kazi yake ambayo aliifanya, na kwa hiyo alipumzika siku ya saba kutoka kwenye kazi yake yote.

Mungu akaibarikia siku ya saba na akaitakasa, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kwenye kazi yake yote ambayo aliifanya katika uumbaji.

Mandhari tulivu alfajiri: simba amelala karibu na kondoo, mbuzi na swala wakipumzika kando ya mto.

Mistari 4–7

Mtu kutoka mavumbini

Haya yalikuwa ni matukio yahusuyo mbingu na nchi, wakati vilipoumbwa, katika siku ambayo Yahwe Mungu aliumba nchi na mbingu.

Hapakuwa na msitu wa shambani uliokuwa katika nchi, na hapakuwa na mmea wa shambani uliokuwa umechipuka, kwa kuwa Yahwe Mungu alikuwa hajasababisha mvua kunyesha juu ya nchi, na hapakuwa na mtu wa kulima ardhi.

Lakini ukungu uliinuka juu kutoka kwenye nchi na kuutia maji uso wote wa ardhi.

Yahwe Mungu aliumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, na akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa kiumbe hai.

Juu ya ardhi nyekundu tupu, mwanaume amelala ndani ya ukungu na mwale wa nuru unashuka juu yake kutoka angani.

Mistari 8 na 9

Bustani katika Edeni

Yahwe Mungu aliotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, na pale akamuweka mtu ambaye alimuumba.

Kutoka ardhini Yahwe Mungu alifanya kila mti uote ambao unapendeza na ni mzuri kwa chakula. Hii ni pamoja na mti wa uzima ambao ulikuwa katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Bustani yenye kustawi inayopitiwa na mto, na miti miwili mikubwa katikati: mmoja unang'aa, mwingine una matunda ya dhahabu.

Mistari 10–14

Mito minne

Mto ukatoka nje ya Edeni kuitia maji bustani. Na kutoka pale ukagawanyika na kuwa mito minne.

Jina la ule wa kwanza ni Pishoni. Huu ni ule ambao unatiririka kupitia nchi yote ya Havila, ambapo kuna dhahabu.

Dhahabu ya inchi ile ni nzuri. pia kuna bedola na jiwe shohamu.

Jina la mto wa pili ni Gihoni. Huu unatiririka kupitia nchi yote ya kushi.

Jina la mto wa tatu ni Hidekeli, ambao unatiririka mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati.

Ramani iliyochorwa ya Mashariki ya Karibu: kutoka bustani katikati, mto unagawanyika kuwa matawi manne yanayotiririka kuelekea baharini. Mto unaotoka Edeni Pishoni Gihoni Hidekeli (Tigri) Frati

Mistari 15–17

Kuilima na kuitunza bustani

Yahwe Mungu alimtwaa mtu na kumweka ndani ya bustani ya Edeni kuilima na kuitunza.

Yahwe Mungu alimuagiza mtu akisema, “kutoka kwenye kila mti bustanini waweza kula kwa uhuru.

Lakini kutoka kwenye mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa kuwa siku utakayo kula kutoka katika mti huo, utakufa hakika.”

Mtu anapogoa mtini karibu na kijito; kwa mbali kuna mti wenye matunda ya dhahabu.

Mistari 18–20

Majina ya wanyama

Kisha Yahwe Mungu akasema, “siyo jambo jema kwamba mtu huyu lazima awe pekeyake. Nitamfanyia msaidizi anaye mfaa.”

Kutoka ardhini Yahwe Mungu akafanya kila mnyama wa kondeni na kila ndege wa angani. Kisha akawaleta kwa mtu huyu aone angewapatia majina gani. Jina ambalo mtu huyu alimwita kila kiumbe hai, hili ndilo lilikuwa jina lake.

Mtu huyu akawapatia majina wanyama wote, ndege wote wa angani, na kila mnyama wa mwitu. Lakini kwa mtu mwenyewe hapakuwa na msaidizi wa kumfaa yeye.

Akiwa amesimama juu ya mwamba, mtu anainua mkono huku simba, ng'ombe, kondoo, farasi, dubu, swala na ndege wakipita mbele yake.

Mistari 21–25

Mwanamke

Yahwe Mungu akaleta usingizi mzito kwa mtu huyu, kwa hiyo mtu huyu akalala. Yahwe Mungu akatwaa moja ya mbavu za mtu huyu na akapafunika pale alipo chukua ubavu.

Kwa ubavu ambao Yahwe Mungu alichukua toka kwa mtu huyu, akafanya mwanamke na akamleta kwa mtu huyu.

Mwanaume akasema, “kwa sasa, huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. ataitwa 'mwanamke,' kwa sababu ametwaliwa katika mwanaume.

Kwa hiyo mwanaume atawaacha baba yake na mama yake, ataungamanika na mke wake, na watakuwa mwili mmoja.

Wote wawili walikuwa uchi, mwanaume na mke wake, lakini hawakuona aibu.

Akiamka chini ya mti wa bustani, mwanaume anamwona mwanamke amesimama mbele yake; wanatazamana kwa furaha.